Deuteronomy 10

Vibao Vingine Vya Amri Kumi

(Kutoka 34:1-10)

1 aWakati ule Bwana aliniambia, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza uje kwangu juu mlimani. Pia utengeneze Sanduku la mbao. 2 bNitaandika juu ya vibao maneno yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza, ambavyo ulivivunja. Kisha utaviweka ndani ya Sanduku.”

3 cHivyo nikatengeneza Sanduku kwa mti wa mshita, nikachonga pia vibao vya mawe kama vile vya kwanza, kisha nikakwea mlimani nikiwa na vibao viwili mikononi mwangu. 4 d Bwana akaandika juu ya hivi vibao kile alichokuwa amekiandika kabla, Amri Kumi alizokuwa amewatangazia juu mlimani, kutoka kwenye moto siku ile ya kusanyiko. Bwana akanikabidhi. 5 eKisha nikashuka kutoka mlimani na kuweka vibao ndani ya Sanduku nililokuwa nimelitengeneza, kama Bwana alivyoniagiza, navyo viko huko sasa.

6 f(Waisraeli walisafiri kutoka visima vya Yaakani hadi Mosera. Huko Haruni alifariki na kuzikwa, naye Eleazari mwanawe akachukua nafasi yake kama kuhani. 7 gKutoka pale, walisafiri hadi Gudgoda wakaendelea mpaka Yotbatha, nchi yenye vijito vya maji. 8 hWakati huo Bwana aliteua kabila la Lawi kulibeba Sanduku la Agano la Bwana, kusimama mbele za Bwana ili kutoa huduma, na kutangaza baraka kwa Jina lake, kama wanavyofanya mpaka leo. 9 iHiyo ndiyo sababu ya Walawi kutokuwa na sehemu wala urithi miongoni mwa ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama Bwana Mwenyezi Mungu wao alivyowaambia.)

10 jBasi nilikaa mlimani kwa siku arobaini usiku na mchana, kama nilivyofanya mara ya kwanza, pia Bwana alinisikiliza hata wakati huu. Haikuwa nia yake kuwaangamiza. 11Bwana akaniambia, “Nenda, ukawaongoze watu katika njia yao ili kwamba waweze kuingia na kuimiliki nchi ile niliyowaapia baba zao kuwapa.”

Mche Bwana

12 kNa sasa, ee Israeli, Bwana Mwenyezi Mungu wako anataka nini kwako ila kumcha Bwana Mwenyezi Mungu wako, kwenda katika njia zake, kumpenda na kumtumikia Bwana Mwenyezi Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote, 13 lna kuyashika maagizo ya Bwana na amri zake ninazokupa leo kwa mafanikio yako mwenyewe?

14 mMbingu, hata mbingu za juu sana, dunia na kila kitu kilichomo ndani yake, ni mali ya Bwana Mwenyezi Mungu wako. 15 nHata hivyo Bwana alikuwa na shauku na baba zako, akawapenda na akawachagua ninyi, wazao wao, kuliko mataifa yote, kama ilivyo leo. 16 oKwa hiyo tahirini mioyo yenu, na msiwe na shingo ngumu tena. 17 pKwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu wenu ni Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye uweza na wa kutisha, ambaye hana upendeleo na hapokei rushwa. 18 qHuwapigania yatima na wajane, humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi. 19 rNanyi wapendeni wageni, kwa kuwa ninyi wenyewe mlikuwa wageni huko Misri. 20 sMche Bwana Mwenyezi Mungu wako na umtumikie yeye. Shikamana naye kwa uthabiti na kuapa kwa jina lake. 21 tYeye ni sifa yako; yeye ni Mungu wako, ambaye alikutendea yale maajabu makubwa na ya kutisha uliyoyaona kwa macho yako mwenyewe. 22 uBaba zako walioshuka kwenda Misri jumla yao walikuwa sabini, na sasa Bwana Mwenyezi Mungu wako amekufanya wengi kama nyota za angani.
Copyright information for SwhKC